Mgonja: Akwaa balaa Keko
2008-12-16 19:03:38
Na Emmanuel Lengwa, Jijini
Ikiwa leo ni siku ya kwanza tangu aliyekuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha Gray Mgonja kutupwa mahabusu Keko,baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana aliyopewa na Hakimu Mkazi Kisutu, kigogo huyo amejikuta akipata pigo jingine akiwa hukohuko lupango.
Pigo hilo ambalo limemkuta huko huko Keko ni taarifa mbaya kwamba, licha ya kutumikia umma kwa miaka chungu nzima, kuna uwezekano wa kupoteza haki zake zote iwapo atapatikana na hatia kwenye kesi iliyofunguliwa dhidi yake.
Mgonja ambaye alipandishwa kizimbani pale Kisutu jana kukabiliana na mashtaka ya kutumia madaraka yake vibaya na kulisababishia taifa hasara ya zaidi ya Sh. Bilioni 11, imedaiwa kuwa kwa vile kesi hiyo imemkumba akiwa likizo ya kujiandaa kustaafu, atakuwa akiambulia sehemu tu ya mshahara wake wa kuwa mtumishi wa umma.
Aidha, imedaiwa vilevile kuwa kwa mujibu wa sheria za utumishi, ni kwamba sasa Katibu Mkuu huyo wa zamani atachelewa kupata mafao yake ya kustaafu hadi kesi yake hiyo itakapokwisha na uamuzi kutolewa.
``Kama asingekumbana na kesi hii, ni wazi kwamba angeweza kupata mafao yake katika kipindi kifupi kulinganisha na sasa ambapo itabidi asubiri hadi kwisha kwa kesi,`` imeelezwa na mtaalam mmoja wa sheria za kazi.
``Na ikitokea kuwa akapatikana na hatia, kuna hatari ya kupoteza mafao yake yote... hili nalo ni pigo jingine zito,`` amedai mwanasheria huyo.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Kitivo cha Sheria, Dk. Sengondo Mvungi, ameiambia Alasiri leo asubuhi kuwa baada ya Mgonja kufikishwa mahakamani hapo jana, inabidi sasa taratibu zote za kisheria zifuatwe juu yake.
Akasema kwa mujibu wa sheria zilizopo, kuanzia sasa Katibu huyo wa zamani wa Wizara ya Fedha ataanza kulipwa nusu tu ya mshahara wake hadi tarehe yake ya kustaafu itakapofika.
Akifafanua zaidi, Dk. Mvungi akasema baada ya muda wake wa utumishi kumalizika, Mgonja hataambulia hata hiyo nusu ya mshahara wake na hivyo kubaki akisubiri hatma ya kesi yake.
Dk. Mvungi ameongeza kuwa endapo Mgonjwa atashindwa kesi hiyo, atakuwa pia amepoteza haki zake zote alizostahili kulipwa kama mafao yake ya kustaafu.
``Akishindwa kesi, mafao yake yote yatakuwa yamepotea kwa mujibu wa sheria,`` akasema.
Jana Mgonja alifikishwa katika mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na kusomewa mashtaka manane yanayohusiana na matumizi mabaya ya madaraka, mbele ya Hakimu Hezron Mwankenja.
Mgonja alisomewa mashtaka hayo na Wakili Mwandamizi wa wa Serikali, Fredrick Mayanda, aliyedai kuwa kati ya mwaka 2003 na 2005, Mgonja akiwa mtumishi wa Umma kama Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha, alipuuza mapendekezo ya Mamlaka ya Mapato Tanzania, TRA na kusamehe kodi kwa kampuni ya Alex Stewart (ASSAYERS) Government Corporation na kulisababishia taifa hasara ya zaidi ya Sh. Bilioni 11.7.
Baada ya kusomewa mastaka yake, Mgonja alikanusha tuhuma zote, na upande wa mashtaka ukadai kuwa hauna pingamizi la dhamana, kabla Hakimu Mwankenja hajatoa masharti ya dhamana yaliyomshinda mtuhumiwa huyo, hivyo kujikuta akisukumwa mahabusu.
Masharti ya dhamana yalkiyotolewa na Hakimu Mwankenja ni pamoja na kujidhamini mwenyewe kwa fedha taslimu Shilingi Bilioni 5.9 au hati ya mali yenye thamani ya fedha hiyo, kuwa na wadhamini wawili, kuwasilisha hati ya kusafiria mahakamani na kutotoka nje ya Mkoa wa Dar es Salaam.
No comments:
Post a Comment