JK aifagilia Taifa Stars licha ya kutolewa CHAN

RAIS Jakaya Mrisho Kikwete ameipongeza timu ya soka ya taifa, Taifa Stars, kwa mafanikio iliyoyapata katika Mashindano ya Ubingwa wa Afrika (CHAN) pamoja na kwamba Stars ilitolewa kwenye mashindano hayo usiku wa jana, Jumamosi, Februari 28, 2009.
Rais Kikwete amesema kuwa amefurahishwa sana na maendeleo ambayo Tanzania imepata katika soka.
Rais Kikwete pia amewapongeza Watanzania kwa kuiunga mkono timu hiyo, na pia amewapongeza makocha wa timu hiyo kwa kazi nzuri waliyoifanya kuinua kiwango cha timu hiyo.
Aidha Rais ameahidi kuendelea kuiunga mkono “timu yetu mpaka tufike pale tunapopata sote” na pia ameupongeza uongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa uongozi wao mzuri katika suala hilo.
Rais amesema kuwa amesikitishwa sana na Taifa Stars kutolewa dakika za mwisho na za majeruhi za mechi ya jana usiku kati yake na timu ya taifa ya Zambia, Chipolopolo katika mechi hiyo iliyochezwa mjini Bouake, nchini Ivory Coast ambako CHAN yanafanyika.
Timu hizo zilitoka sare 1-1 na hivyo kuifanya Taifa Stars kuikosa nafasi ya kucheza nusu fainali kwa unyoya tu.
Stars imemaliza mechi zake ikiwa na pointi nne baada ya kuwashinda wenyeji Ivory Coast 1-0, ikatoka sare na Zambia 1-1 na kufungwa 1-0 na Senegal.
Nchi za Zambia na Senegal zimesonga mbele kutoka kundi hilo kwa kupata pointi tano kila moja.
Hadi dakika ya 90 za mechi ya jana, Taifa Stars ilikuwa inaongoza kwa bao 1-0 lililofungwa kwa penelti katika dakika ya 87 na nahodha wa timu hiyo, Sahdrack Nsajigwa baada ya mlinzi mmoja wa Chipolopolo kuunawa mpira katika eneo la penelti.
Mwamuzi wa mechi hiyo aliongeza dakika tano baada ya kumalizika kwa muda wa kawaida wa mchezo, na Rais Kikwete amesema: “Nimesikitika sana tumetolewa dakika za majeruhi.”
Lakini ameongeza Rais ambaye amekuwa shabiki nambari moja wa Taifa Stars: “ Lakini nimefurahi sana kwa hatua tulifikia katika maendeleo ya soka. Sasa tunatambulika na kuheshimika katika ulimwengu wa soka Barani Afrika.”
Ameongeza Rais: “Tuongeze bidii, tusirudi nyuma, bali twende mbele.
Nawapongeza wachezaji kwa juhudi zao. Nawapongeza walimu kwa kazi waliyoifanya kuinua kiwango cha soka nchini. Nawapongeza viongozi wa TFF kwa uongozi wao mzuri.”
Kuhusu Watanzania, Rais amesisistiza: “Nawapongeza Watanzania kwa kuiunga mkono timu yenu. Mmekuwa chachu ya mafanikio hayo. Watanzania wenzangu tufe moyo, mwanzo mgumu. Tumeanza vizuri na tumefika pazuri. Tuendelee kuiunga mkono timu yetu.”
Kuhusu ahadi yake kwa timu hiyo, Rais amewahakikishia wachezaji wa timu hiyo na Watanzania wote: “ Mimi naahidi kuendelea kuiunga mkono timu yetu mpaka tufike pale tunapopata sote.”
Mashindano ya CHAN yanashirikisha wachezaji wanaocheza katika ligi za soka za nyumbani Barani Afrika, na hii imekuwa mara ya kwanza kwa Tanzania kufanikiwa kuingia katika fainali za Kombe la Afrika katika miaka 28.
Mara ya mwisho, Tanzania ilifikia hatua hiyo ilikuwa mwaka 1980 katika mashindano yaliyochezwa Lagos, Nigeria. Kwa namna pekee ya kihistoria, Tanzania iliingia fainali za 1980 kwa kuitoa Zambia.
Katika hotuba yake ya Desemba 30, mwaka 2005, baada ya kuwa ameapishwa kuwa kuongoza Tanzania, Rais Kikwete aliahidi kuendeleza michezo na katika moja ya hatua zake kufanikisha dhamira hiyo ilikuwa ni kuajiri kocha wa kulipwa wa Taifa Stars, Marcio Maximo kutoka Brazil ambaye ameinua sana kiwango cha Stars.
No comments:
Post a Comment