Jeshi la Polisi lajipanga upya kudhibiti ujambazi
2008-12-16 19:07:57
Na Sharon Sauwa, Jijini
Jeshi la Polisi nchini limeanza program maalum ya kutumia helkopta, boti, magari na pikipiki katika kuwasaka majambazi na wahalifu wengine popote walipo nchini na kuwakamata.
Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, Kamishna Msaidizi Abdallah Masika, ameliambia Alasiri leo asubuhi kuwa programu hiyo imeanza jana katika mikoa ya Dar es Salaam na ile inayolizunguka Jiji hilo.
Akaitaja mikoa hiyo kuwa ni pamoja na Morogoro, Pwani, Tanga, Unguja na Pemba.
``Kama wananchi walivyoona, tumeanza jana ambapo helkopta za polisi na boti zimekuwa zikizunguka katika maeneo mbalimbali kwa ajili ya doria za kuwasaka wahalifu,`` akasema Kamishna Masika.
Akasema ndani ya boti hiyo kuna askari wa vikosi maalum vya kuzuia uhalifu ambao wamekuwa wakiwasiliana na askari wa doria wa nchi kavu kila mara.
Kamishna Msaidizi huyo akawataka wananchi ambao wana taarifa kuhusiana na uhalifu kuwasiliana na jeshi hilo ili kudhibiti mapema njama za uhalifu.
``Hawa wahalifu ni watoto wetu, ndugu zetu, jirani zetu lazima tuelewe kuwa hili ni janga la kitaifa...tuwafichue,`` akasema.
Akasema wameona mafanikio baada ya kuanza zoezi hilo ambapo hawajapata taarifa ya tukio lolote kubwa la uhalifu lililojitokeza katika muda huo.
``Kwa muda wa saa 24 zilizopita hadi sasa, hatujapata taarifa ya tukio lolote kubwa la uhalifu,`` akasema.
Akasema programu hiyo inajumuisha maeneo ya mipakani ambapo askari wa doria (wanaotumia miguu), pikipiki, magari, vikosi vya mbwa na farasi vimekuwa vikifanya doria za kusaka wahalifu.
Akasema programu hiyo itakuwa endelevu, ikiwa ni mpango ulioandaliwa nchini kwa ajili ya kupambana na uhalifu nchini.
Wiki iliyopita, Jiji la Dar es salaam lilikumbwa na mfululizo wa matukio ya ujambazi ambapo mojawapo ni lile la mhasibu wa kituo cha Mafuta cha Gapco Magomeni aliuawa kwa kupigwa risasi na kisha majambazi hao kutimka na mamilioni ya pesa.
No comments:
Post a Comment