EPA: Ni hatari!
2008-11-15 16:38:22
Na Emmanuel Lengwa, Jijini
Siku moja tu baada ya mahakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kutaka wahakikishiwe ulinzi kutokana na hatari wanayohisi kuweza kukumbana nayo wakati huu wakiendesha kesi ihusuyo wizi wa mabilioni ya pesa za EPA, Jeshi la Polisi limestuka na sasa limemwaga askari kibao kwa ajili ya kuzima hofu hiyo.
Aidha, jeshi hilo kupitia Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna Suleiman Kova, limedai kuwa sasa askari wake wataongeza ulinzi pale katika Mahakama ya Kisutu na pia kwingineko Jijini, wakitumia mbinu zao mbalimbali za kipolisi.
Kamanda Kova ameiambia Alasiri leo asubuhi kuwa wao wamepata taarifa za kuwepo kwa hofu hiyo ya hatari itokanayo na usikilizwaji wa kesi za watuhumiwa wa EPA na kwamba kwa sababu hiyo, tayari wameanza kuchukua hatua ya kuhakikisha kuwa ulinzi na usalama unaimarishwa katika kila eneo.
Kamanda Kova ametoa ufafanuzi huo baada ya kuwepo taarifa ya hofu kuwa wapo baadhi ya watu wanaoonekana kuwa tishio kwa usalama wa mahakimu, makarani na wadau wengine wanaoshughulikia kesi hiyo ya EPA.
Aidha, imedaiwa kuwa wapo jamaa ambao wanahisiwa kuwafutilia watumishi hao wa umma hadi maeneo ya majumbani kwa nia ya kuwatisha, jambo ambalo hata hivyo, Kamanda Kova amesema jeshi lake limejipanga katika kuhakikisha kuwa usalama ni wa hali ya juu katika kila eneo Jijini.
Kamishna Kova amesema hivi sasa, tayari ameshamuagiza Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, kuimarisha ulinzi katika eneo la Mmahakama ya Kisutu.
Akasema vilevile kuwa jeshi lake linaimarisha ulinzi katika sehemu nyinginezo ambazo wanahisi kuwa baadhi ya watuhumiwa hao au ndugu zao wanaweza kupata nafasi ya kuleta vitisho.
``Tumeanza kuweka ulinzi Kisutu na sehemu nyingine ambazo ni tishio kwa mahakimu na wafanyakazi wengine wa mahakama hiyo,`` akasema Kamanda Kova.
``Wafanyakazi wote wawe na ujasiri, wafanye kazi zao bila woga kwa sababu Serikali ipo na polisi inawahakikishia usalama wao wakati wote,`` akasema Kamanda Kova.
Kama hiyo haitoshi, Kamanda Kova akasema Polisi tayari imeanza kuwachunguza watu wanaodhani wanaweza kuwa tishio kwa wafanyakazi wa mahakama hiyo wakiwemo ambao ni pamoja na mahakimu na makarani.
Akasema ikiwa watabainika kuwa wanafanya vitendo vinavyohatarisha usalama wa wafanyakazi wa mahakama hiyo watakamatwa na kushughulikiwa kwa mujibu wa sheria.
``Tunachunguza yeyote tunayedhani anaweza kuhatarisha usalama wa wafanyakazi hao... tukimbaini, tutamkamata kabla hajatekeleza uhalifu wake na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria. Nasisitiza kuwa wafanyakazi wasiwe na wasiwasi,`` akasema Kamanda Kova.
Hata hivyo, Kamanda Kova akawataka mahakimu na makarani wa mahakama hiyo, kama walivyo binadamu wengine wa kawaida, nao wachukue tahadhari ya usalama wao na kutoa taarifa polisi pindi wakihisi kuna jambo lisilo la kawaida.
Akasema ikiwa watahisi kuna mtu anawafuatilia au kuhatarisha usalama wao, wanapaswa kuchukua hatua za haraka za kuliarifu Jeshi la Polisi ili hatua zichukuliwe.
Leo, imeripotiwa kuwa mahakimu wanaoshughulikia kesi maarufu ya wizi wa pesa zilizokuwa Benki Kuu (BOT), kupitia Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje, EPA wamekuwa wakihofia usalama wao kutokana na sababu kadhaa ikiwemo ya ulinzi.
No comments:
Post a Comment