ajali ajali ajali ajali ajali...
Watu 15 wamekufa katika ajali zilizohusisha magari na treni katika mikoa ya Dar es Salaam na Morogoro, huku zikiacha majeruhi zaidi ya 20.
Katika ajali hizo mbili zilizotokea alfajiri ya kuamkia jana; mkoani Dar es Salaam, watu tisa walikufa papo hapo na wengine 10 kujeruhiwa katika eneo la Jet Club, Kipawa, barabara ya Nyerere wakati Morogoro, watu sita walikufa papo hapo na wengine 10 kujeruhiwa katika ajali ya treni la Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) kati ya stesheni za Mzaganza na Kidete, Kilosa.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema jana kuwa ajali ya Kipawa ilitokea saa 10 alfajiri baada ya gari namba T 700 AFT aina ya Toyota Hiace ‘Kipanya’ lililokuwa likitoka Uwanja wa Ndege wa JK Nyerere, kwenda Tazara, kugonga lori namba T 452 ACP aina ya Scania lililokuwa limeanguka katikati ya barabara na kusababisha kifo cha abiria tisa papo hapo.
Aliwataja baadhi ya waliokufa kuwa ni Ally Issa (37), Michael Maujiro, Augustino Yohana, Elly Athumani, Alphonce Golesh, Machel Msagira (33) na John Steven.
Alisema maiti wamehifadhiwa katika Hospitali ya Amana wakati majeruhi 10 wamelazwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa matibabu.
Alisema chanzo cha ajali hiyo, ni mwendo kasi wa dereva wa Hiace ambayo ilikuwa na abiria ikitoka Machinjioni Pugu. Ilibainika kuwa gari hilo lilikuwa linafanya kazi usiku tu kutokana na muda wa leseni yake kumalizika.
Naye Ofisa Habari Msaidizi wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI), Mary Ochieng, alisema hali za majeruhi hao zinaendelea vizuri kiasi.
“Tunaendelea kuwapa matibabu … mmoja bado yuko ICU (chumba cha uangalizi maalumu) na tayari tumesharuhusu wawili,” alisema Ochieng jana mchana.
Waliolazwa ni Simon Sylvester (27), Eva Joseph (28), Kalunde Osambi (32), Zamoyoni Mongella (36), Joshua Jumanne (29), Alex Msuya (65), Emilly Steven (40) na Ratibu Abdallah (21).
Ajali ya Morogoro, ilitokea saa saba usiku wa kuamkia jana, ikihusisha treni namba 8828 lililokuwa likiendeshwa na Richard Mkude (38) kwa kushirikiana na Lucas Isaya, wote wakazi wa Morogoro.
Treni hiyo iliyokuwa na mabehewa manne, ilikuwa ikitoka Bara kwenda Dar es Salaam. Kamanda wa Polisi wa Kikosi cha Reli, Yessaya Msigwa, alithibitisha ajali hiyo na akizungumza kwa simu akiwa eneo la tukio, alisema katika mabehewa hayo manne, moja lilikuwa la abiria, jingine tupu wakati jingine lilibeba mataruma kutoka Mpanda, Rukwa.
Alisema lilipofika Mzaganza, behewa moja la nyuma liliyumba na kufuatiwa na lenye abiria na yote kupinduka na kusababisha vifo hivyo na majeruhi hao waliokuwa wakitoka mnadani.
Kamanda Msigwa aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni wafanyabiashara Said Pindupindu, Seif Bakari, Nassoro Mohamed, Jonas Lukanda, Abbas Kandaro; wote kutoka Wilaya ya Kilosa na mwingine mmoja ambaye jina lake halijatambuliwa.
Aliwataja waliojeruhiwa katika ajali hiyo na kulazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kilosa ni Hamisi Chamwitu, Seleman Mohamed, Sadik Monera, Esther Mbwambo na Asha Hamis wakazi wa Morogoro.
Wengine waliolazwa katika hospitali hiyo ni Edward Athanas, Aziz Seleman wote wa Dar es Salaam; Hamis Manyeleta, Hamis Selemani na Mecha Jackson wa Kilosa. Kamanda alisema marehemu wamehifadhiwa katika mochari ya Hospitali ya Kilosa.
Alisema kazi ya kutambua miili hiyo ilikuwa ikiendelea na hadi jana mchana, maiti watano kati ya sita walikuwa wameshatambuliwa na ndugu zao na majeruhi wanaendelea vizuri.


No comments:
Post a Comment