Anna Abdallah apasua fataki uchaguzi UWT
2009-01-08 12:03:42
Na Mary Edward, Dodoma
Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) anayemaliza muda wake, Anna Abdallah, amesema wagombea wa nafasi ya uenyekiti katika uchaguzi wa jana ulitawaliwa na vitendo vya rushwa na kupakana matope.
Akizungumza kabla ya kufunguliwa kwa mkutano huo, Anna alisema kuwa UWT iliwakataza kabisa wagombea kupita mikoani kuomba kura nje ya vikao vya uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kutochapisha vipeperushi vya kampeni na kugawa vijizawadi kwa nia ya kuwashawishi wapiga kura, lakini hawakutii.
``Wagombea walitii, lakini kuna wapambe nuksi, ambao wamezunguka mikoani kwa gharama kubwa, huku baadhi ya watendaji wa UWT wakihusika kuandaa mikutano ya wapambe hao na kutumia ofisi za Chama katika kuwanadi wagombea wao,`` alisema Anna.
Alifafanua kuwa wapambe hao hawakuishia hapo bali waliendelea kuendesha kampeni chafu za kashfa na za kupakana matope na wengine kudiriki hata kusema eti mgombea wao ndiye anayetakiwa na Makao Makuu ya UWT.
Aliongeza kuwa wapambe wengine walidai kuwa mgombea wao ni chaguo la CCM na kutumia mitandao ya simu kuwatumia ujumbe wa vitisho wajumbe wenzao wasiokubaliana na mgombea wao.
``Karibu wajumbe wengi hapa wamewaona wapambe hao mikoani na wengine wamepokea vitisho katika simu zao. Naomba kuwaasa wajumbe kwamba wapambe hao ni hatari kuliko virusi vya Ukimwi…tunawalaani kwani hao ndio wanaopandikiza chuki baina ya wanachama,`` alisisitiza Anna.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alimweleza mgeni rasmi katika mkutano huo, Mwenyekiti wa CCM, Jakaya Kikwete, kuwa kuna jambo ambalo limeanza kujitokeza kwa wenyeviti wa UWT wa mikoa na wilaya, ambao wametuma taarifa makao makuu wakidai kuwa hawawataki makatibu wao, kwa madai kuwa hawakushiriki katika kampeni zao za uchaguzi.
Anna aliwapongeza watendaji wa UWT ambao hawakujiingiza katika makundi ya uchaguzi, kwamba wao walijiweka katika hali ya kufanya kazi na yeyote atakayeshinda.
``Kama mtendaji hatoshi basi ajadiliwe katika vikao na ahukumiwe kwa makosa yake, lakini yasiwe ni matakwa ya mtu au kikundi cha watu, vinginevyo tutawapoteza watendaji wazuri, na wapo baadhi ya wapambe wamesikika wakisema mgombea wao akishinda, basi kuna makatibu wataipata,`` alisema.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyo alisema pamoja na mafanikio yaliyoonekana katika kumsaidia mwanamke, bado kuna vikwazo vingi ambavyo vimekuwa vikimkwamisha kushika nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya serikali.
Alivitaja vikwazo hivyo kuwa ni pamoja na baadhi ya wanaume na wanawake wasiokubali mabadiliko, ambao huwakatisha tamaa wanawake na kusababisha wasishinde katika nafasi wanazogombea.
Vikwazo vingine alisema ni pamoja na baadhi ya wanachama ndani ya CCM kufikiri kuwa wana hati miliki ya uongozi na hivyo kuwazuia wengine kushika nyadhifa hizo.
Vilevile, alizungumzia matumizi makubwa ya fedha kwenye uchaguzi, akisema kumekuwa na uongozi wa kununuliwa ndani ya chama na kama mgombea huna fedha, hata wale wasikokuwa na fedha zao kuna watu au vikundi vinavyotoa fedha kwa niaba yake.
Akiufungua mkutano huo, Rais Kikwete alisema umefika wakati kwa CCM kufanya mabadiliko kwa kuwa na viongozi wasomi.
Alisema kutokana na changamoto mbalimbali zinazojitokeza hivi sasa duniani za mabadiliko ya sayansi na teknolojia, itakuwa ngumu kwa viongozi wasio na elimu kukabiliana na changamoto hizo.
``UWT lazima ifanye juhudi katika kuhakikisha kuwa inakuwa na viongozi wasomi, tusipowekeza katika elimu katika karne hii ya sayansi na teknolojia na kuwa na wasomi wa kutosha, watatupuuza,`` alisema.
Aliwataka wajumbe wawe makini katika kuchagua viongozi wenye sifa, ili wasije kujutia kwa miaka mitano ya uongozi wa Jumuia hiyo.
``Chagueni viongozi madhubuti na wachapakazi, wapo mtakaokuwa nao kwa jua na mvua, kwa shida na raha... tunataka viongozi watakaoifaa UWT na sio kwa sababu wanakufaa wewe,`` alisema Mwenyekiti huyo wa CCM na kuongeza: ``Anayekufaa wewe ni mumeo na ndugu zako.``
Aliwatahadhalisha wajumbe wasichague viongozi kwa kuwa ni mashoga zao, au kwa kuwa wanawafadhili au kuwapa kitu chochote kwani hivyo sio vigezo vya kiongozi.
Aidha, aliwataka wajumbe hao kuwapima wagombea kama wanafaa kuyakabili majukumu ya Umoja huo ili kudumisha mshikamano na umoja.
``Muwapime wagombea kwa kufaa kwao, hata kama ni rafiki yako ukiona hana sifa hizo mwambie kwamba sitakuchagua kwa vile nimeona huna sifa hizo,`` alisema.
Rais Kikwete pia aliwabeza baadhi ya wanachama ambao tabia zao na vitendo vyao haviwakilishi CCM.
``Kuna baadhi ya wanachama humu hata wakisimama jukwaani kuisemea CCM wanawashanga kwa sababu wanayoyafanya hayawakilishi Chama Cha Mapunduzi,`` alisema.
Kuhusu tatizo sugu la mimba kwa wanafunzi wa kike, aliutaka Umoja huo kusimama kidete kuhakikisha tatizo hilo linakomeshwa.
Alisema serikali inaendelea kujenga hosteli katika shule za sekondari ili kuhakikisha wanafunzi wote wa shule za sekondari wanaishi kwenye hosteli na kuondokana na vitendo vya kurubuniwa na wanaume pale wanapopanga kwenye vyumba mitaani.
Akizungumzia ufisadi, Rais alisema wapo wanaomsakama ataje majina ya mafisadi hadharani, aliwataka wamuache kwa sababu vyombo vya sheria vipo na vinaendelea kuwachunguza na kuwafikisha mahakamani.
Alisisitiza kuwa anataka kila mtuhumiwa wa ufisadi atendewe haki badala ya kuchukua hatua kwa kutumia chuki binafsi. Alisema baada ya vyombo hivyo kuwachunguza na kuwabaini, watatajwa hadharani kama walivyotajwa wengine.
``Nafahamu wapo watu wanaonitaka mimi niwataje kwa majina watu wanaohusika na ufisadi, jamani suala hapa sio kutaka kumdhalilisha mtu, bali tunataka haki itendeke kwa kila mmoja, ndio maana vipo vyombo vya sheria, ambavyo vimekabidhiwa jukumu hilo.
Watakapochunguza na kubaini ukweli, watu hao watatajwa hadharani na kuchukuliwa hatua, kama walivyochukuliwa hatua watuhumiwa wengine,`` alisisitiza Rais Kikwete.
No comments:
Post a Comment