Thursday, January 8, 2009

ewura

VIVA LE TANZANIA

Ewura yazidi kutwanga maji kwenye kinu

2009-01-08 12:02:07
Na Abdallah Bawazir

Huku makampuni ya kuuza mafuta yakiendelea kukaidi agizo la Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) la kuyataka yashushe bei ya nishati hiyo, mamlaka hiyo imeshusha zaidi bei ya bidhaa hiyo na sasa imeweka utaratibu wa kutangaza bei mpya kila wiki, kulingana na mwenendo wa soko la mafuta duniani.

Taarifa iliyotolewa na Ewura jana ilieleza kuwa kutokana na bei ya mafuta kuendelea kushuka katika soko la dunia, mamlaka hiyo imelazimika kushusha zaidi bei ya mafuta kwa soko la ndani ili kuweka uwiano wa haki wa kibiashara kati ya wafanyabiashara na watumiaji.

Wiki iliyopita, Ewura ilitangaza bei ya mafuta ya petroli na dizeli ambazo vituo vyote vinavyouza bidhaa hiyo nchini vitalazimika kuzifuata, baada vituo hivyo kushindwa kushusha bei licha ya bei kushuka kwa kiasi kikubwa katika soko la dunia.

Katika agizo hilo lililotolewa na Ewura kupitia Mkurugenzi Mkuu wake, Haruna Masebu, Ijumaa ya wiki iliyopita, makampuni hayo yalitakiwa kuanzia Jumatatu ya wiki hii yaanze kuuza petroli kwa bei ya kati ya Sh1,166 na Sh1,249, wakati dizeli yalitakiwa yauze kwa Sh.1,367 na Sh.1,469 na mafuta ya taa Sh.814 na Sh.875 kwa lita moja kwa mkoa Dar es Salaam.

Awali, kabla ya kutolewa kwa agizo hilo, bei ya mafuta ilitofautiana kati ya kituo kimoja na kingine ingawa vituo vingi viliuza nishati hiyo kwa kati ya Sh.1,600 na Sh.1,700 na dizeli Sh.1,700 na Sh.1,750 kwa mkoa huo.

Hata hivyo, makampuni hayo hadi sasa yameigomea serikali baada ya kukaidi agizo la kushusha bei ya nishati hiyo, hivyo kuendelea kuuza kwa bei ya juu.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe katika baadhi ya vituo vya kuuzia mafuta jana jijini Dar es Salaam umebaini kuwa agizo hilo halijatekelezwa, badala yake makampuni hayo yameendelea kuuuza kwa bei ya juu.

Katika uchunguzi huo, ni vituo vichache peke ndivyo vilivyobainika kuitikia wito wa Ewura kwa kushusha mafuta ya dizeli pekee, lakini petroli na mafuta ya taa, vimeendelea kuuza kwa bei ya juu.

Aidha, uchunguzi umebaini kuwa katika vituo vingi vya mafuta mabango yanayopasa kueleza bei ya mafuta, hakuna bei iliyobandikwa na badala yake yanasomeka 0000.

Baadhi ya wateja waliokuwa wakifika katika vituo hivyo vya mafuta walionekana kupigwa butwaa baada ya kuona kuwa bei za mafuta hazina mabadiliko kama ambavyo serikali imeagiza.

Wakati makampuni hayo yakiendelea kukaidi agizo hilo la Ewura, mamlaka hiyo imeibuka tena na kushusha rungu jingine kwa wafanyabiashara ya mafuta, kwa kuwataka washushe zaidi bei kwani bei katika soko la dunia kwa wiki hii imeshuka zaidi.

Taarifa mpya kwa umma iliyotolewa jana na Ewura kuhusu bei za mafuta aina ya petroli, ilionyesha kuwa vituo vya mafuta vinatakiwa kushusha tena bei.

Hata hivyo, taarifa hiyo inayoonyesha kuwa bei hiyo itashuka kwa kiwango tofauti kutegemea umbali wa eneo husika.

Taarifa hiyo inaonyesha kuwa vituo vya mafuta jijini Dar es Salaam vinatakiwa kuuza petroli kwa bei ya rejareka kati ya Sh 1,147 na Sh. 1,233 badala ya Sh 1,166 na Sh. 1,249 iliyotangazwa wiki iliyopita; mkoa wa Arusha kati ya Sh 1,243 na 1,336 badala ya Sh. 1,262 na 1,345; Dodoma kati ya Sh. 1,216 na 1,303 badala ya Sh 1,235 na 1,318, Iringa kati ya Sh. 1,232 na 1,325 badala ya Sh 1,251 na 1,334.

Bukoba ni kati ya Sh. 1,404 na 1510 badala ya Sh. 1,423 na 1,506; Kigoma Sh. 1,404 na 1,510 badala ya Sh. 1,423 na 1,506; Moshi kati ya Sh. 1,225 na 1,317 badala ya Sh 1,244 na 1,327 na Lindi kati ya Sh. 1,243 na 1,337 badala ya Sh 1,262 na 1,345.

Mbeya Sh 1,243 na 1337 badala ya 1,269 na 1,352; Tanga Sh 1,216 na 1,308 badala ya 1,235 na 1,318; Morogoro Sh 1,185 na 1,274 badala ya 1,204 na 1,287; Mwanza Sh. 1,356 na 1,458 badala ya 1,375 na 1,458; Musoma Sh. 1,387 na 1,491 badala ya 1,406 na 1,489; Babati Sh. 1,263 na 1,358 badala ya 1,282 na 1,365; Mtwara Sh. 1,227 na 1,319 badala ya 1,249 na 1,329; Songea Sh. 1,265 na 1,360 badala ya 1,284 na 1, 253 na 1,366; Singida Sh. 1,235 na 1,327, Shinyanga Sh. 1,279 na 1,375 na Tabora Sh. 1,279 na 1,375.

Kuhusu bei ya mafuta ya taa kwa wiki hii makampuni yanatakiwa kuuza lita moja kwa kati ya Sh. 800 hadi 1,050 badala ya Sh 800 na 1,071 iliyotangazwa wiki iliyopita.

Akizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Wizara ya Nishati na Madini, jijini Dar es Salaam juzi, Waziri wa Wizara hiyo, William Ngeleja alisema serikali iko makini katika suala hilo na kwa hiyo, haitakubali kamwe sababu zozote zitakazotolewa na makampuni hayo kupandisha bei ya mafuta kienyeji.

``Hatua kali zitachukuliwa dhidi ya watakaokaidi na hili hatuna mchezo nalo hata kidogo,`` alisema Waziri Ngeleja alipokuwa akielezea mafanikio yaliyopatikana katika wizara yake pamoja na changamoto zinazoikabili, katika kipindi cha miaka mitatu ya utawala serikali ya awamu nne.

Mkurugenzi Mkuu wa Ewura ameileza Nipashe kuwa kupitia mapendekezo hayo vituo vya kuuza mafuta vitakuwa huru kuuza bidhaa za mafuta kwa bei ya ushindani kwa kuzingatia bei hizo hazizidi bei ya kikomo iliypangwa na mamlaka hiyo.

Alifafanua kuwa bei ya kikomo iliyopangwa ni asilimia 7.5 ya bei elekezi kama ilivyokokotolewa na fomula iliyopitishwa na Ewura.

Alieleza kuwa sheria ya Ewura na Sheria ya Mafuta kama ilivyorekebishwa kwenye Sheria ya Fedha namba 16 ya mwaka 2007 inaipa nguvu mamlaka hiyo kuingilia na kurekebisha mfumo wa uchumi kwa kutoa watoa huduma wanaodhibitiwa kwa lengo la kupunguza mwenendo usiokidhi katika kupanga bei, kupata faida na jinsi ya kufanya manunuzi.

No comments: