VIVA LE TANZANIAMwanafunzi Norbeth Massawe (15) wa shule ya Sekondari Ivumwe jijini Mbeya mwenye ulemavu wa ngozi (Albino) amelilalamikia jeshi la polisi mkoani Mbeya kwamba ni chanzo cha kuchochea mauaji ya albino kutokana na kauli zenye utata za baadhi ya viongozi waandamizi wa jeshi hilo kuwaita albino kuwa ni malighafi na dili.
Mwanafunzi huyo ambaye hivi karibuni alipata mkasa wa kukamatwa na watu wasiojulikana na kumnyoa nywele zote kichwani, ametoa masikitiko hayo juzi wakati wa mahojiano maalum na Nipashe yaliyofanyika katika ofisi ya Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Ivumwe, Nolbert Kaguo.
Alisema mauaji ya kinyama wanayofanyiwa albino kwa kiasi kikubwa yanachangiwa na kauli zenye utata zinazotolewa na baadhi ya viongozi wa serikali, wakiwemo wa jeshi la polisi ambao badala ya kukataza wananchi wasiwaite albino dili lakini wao wenyewe ndio wamekuwa chanzo cha kuendelea na kauli hizo.
Massawe alitoa mfano baada ya kupata mkasa wa kukamatwa na watu wasiojulikana waliomnyoa nywele na kutoweka nazo, aliitwa katika kituo cha polisi ambapo mmoja wa viongozi waandamizi wa polisi alianza kumkemea baba yake kwamba ni mzembe kwa kuwa ameshindwa kumlinda mwanawe huku akijua kuwa hivi sasa albino ni dili na malighafi kubwa hapa nchini.
``Tatizo la mauaji ya albino lingekuwa limekomeshwa muda, lakini serikali yenyewe inaendekeza kwa sababu wanaficha maovu, mfano wakati nikiwa kituo cha polisi kuhojiwa mimi na wazazi wangu Mkuu wa Polisi wa Upelelezi wilaya aliwakemea wazazi wangu kwamba inabidi wafungwe kwa sababu wameshindwa kunilinda huku wakijua kuwa albino hivi sasa ni dili na malighafi kubwa nchini,`` alisema Masawe kwa masikitiko makubwa.
Alisema kauli hiyo ya kiongozi huyo wa polisi ilimkera sana na kupata mawazo kuwa kama viongozi kama hawa wataendelea na kauli za kuwaita albino dili kamwe mauaji ya watu wenye ulemavu wa ngozi hayatakwisha kwa sababu kauli hizo zinahamasisha mauaji hayo.
Mwanafunzi huyo pia alieleza kusikitishwa kwake na kitendo cha baadhi ya maofisa wa polisi Wilaya Mbeya kumuomba rushwa ya Sh. 40,000 baba yake mzazi aliyekamatwa kwa madai kuwa ameshindwa kumlinda na kusababisha watu kumwinda kwa lengo la kutaka kumuua.
Mwanafunzi huyo pia ameiomba mahakama kumfutia kesi baba yake mzazi aliyekamatwa na polisi na kufunguliwa kesi kwa madai kuwa alishindwa kumlinda na kusababisha akamatwe na watu wasiojulikana ambao walimnyoa nywele.
Alisema kimsingi wazazi wake hawajashiriki kupanga njama za yeye kunyolewa nywele kama inavyodhaniwa na baadhi ya watu kwa sababu kama kweli wangekuwa na nia hiyo basi ingekuwa siku nyingi wamepanga njama za kumfanyia tukio lolote baya.
``Wazazi wangu wananipenda sana kamwe hawawezi kushiriki njama za mimi kunyolewa nywele, kama kweli wangekuwa wana nia hiyo basi wangekuwa wamefanya hivyo kwa mdogo wangu mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi miwili aitwaye Sharo ambaye pia ni albino,`` alisema Masawe.
Kamanda wa polisi mkoa wa Mbeya, Zelothe Stephen, hakuweza kupatikana kuelezea malalamiko hayo kwa kuwa yupo safarini ambapo aliyeachiwa ofisi naye alikataa kutoa maelezo yoyote juu ya kauli iliyotolewa na kiongozi mmoja mwandamizi wa polisi.
Hivi karibuni Kamanda Stephen alisema mwanafunzi
huyo, Norbeth Masawe (15), ambaye ni mlemavu wa ngozi alikamatwa na watu watatu wasiojulikana na kumnyoa nywele na kuondoka nazo na kisha kumtelekeza.
Alisema mwanafunzi huyo ambaye anasoma kidato cha kwanza katika shule hiyo, alipata mkasa huo Februari 5, mwaka huu majira ya saa 12:45 alfajiri wakati akiwa njiani kuelekea shule.
Alisema siku ya tukio mwanafunzi huyo akiwa peke yake kuelekea shule, ghafla alikamatwa na watu watatu, wawili kati yao wanaume na mmoja mwanamke waliokuwa wamejificha kwenye tanuri la matofali ambao baada ya kumkamata walitandika mfuko wa plastiki (nailoni) na kumkalisha kwenye tofali na kuanza kumnyoa nywele.
Watu hao baada ya kumaliza zoezi la kumnyoa nywele zote, walimchanja chale mbili mkono wa kushoto na kumpaka masizi meusi na kisha wakamtelekeza hapo na kutokomea kusikojulikana.
Mwanafunzi huyo baadaye aliondoka zake na kwenda shuleni akiwa amevaa kofia na aliporejea nyumbani kwao alitoa taarifa kwa mama yake aliyefahamika kwa jina la Upendo Massawe, ambaye naye alitoa taarifa kwa balozi na ndugu wengine na baadaye taarifa zikatolewa polisi.
Kamanda Stephen alisema kufuatia tukio hilo, aliagiza baba wa mwanafunzi huyo Saimon Masawe (42), pamoja na balozi wa mtaa Ivumwe, Rhoda Mtulo (44), wakamatwe kwa kushindwa kulinda usalama wa mwanafunzi huyo ambao wamefunguliwa kesi mahakamani.
Sunday, March 1, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment