Sunday, March 1, 2009

uhaba waumeme waja

VIVA LE TANZANIAShirika la Umeme Nchini (Tanesco), limetahadharisha nchi inahitaji umeme wa dharura hivyo ni muhimu hatua zichukuliwe kununua mitambo ya Dowans haraka.

Tayari serikali imepingwa vikali na wadau mbalimbali ikiwemo Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini, katika suala zima la kutaka kununua mitambo ya kampuni hiyo.

Taarifa ya Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk. Idrisa Rashid, iliyotolewa jijini Dar es Salaam jana ilieleza kuwa utafiti wa ukuaji wa sekta ya umeme nchini unaonyesha mahitaji ya nishati hiyo yanaongezeka kwa kasi na katika kipindi cha mwaka huu na 2013 kutakuwa na uhaba mkubwa wa umeme.

Katika taarifa hiyo, Dk. Rashid alisema kutokana na kasi ya ongezeko hilo, kuna umuhimu wa kuwa na mashine kubwa kwa ajili ya kukabiliana na dharura itakayojitokeza.

``Kwa sasa mahitaji ya umeme yamefikia megawati 700 na gridi ya taifa haina ziada yoyote hii ina maana kuwa zaidi ya megawati 105 zinahitajika kuongezwa kila mwaka ili kukidhi mahitaji ya umeme katika kipindi hicho ukilinganisha na ukuaji wa mahitaji ya umeme, ambayo ni asilimia 10 hadi 15 kwa mwaka,`` alisema Dk. Rashid katika taarifa hiyo.

Alisema tayari shirika lilishafanya ukaguzi katika mitambo ya Dowans na kubaini kuwa ipo katika hali nzuri.

``TANESCO ilimwajiri mtaalam kutoka kampuni ya Lahmeyer International ya Ujerumani kwa ajili ya kukagua mitambo yote ya Dowans...kwa ufupi matokeo ya ukaguzi huo ni kwamba mashine zote nne ziko kwenye hali nzuri kwa uzalishaji zaidi. Kulingana na hali hiyo, mtaalam huyo alikadiria thamani ya mashine na vifaa kuwa nafuu zaidi kuliko gharama za mitambo mipya,``alisema.

Dk. Rashid alisema shirika lake linaishauri serikali kununua mtambo huo pamoja na vifaa vyake vyote vya kuunganishia kwenye gridi ya taifa.

Alisema iwapo serikali itashindwa kununua mtambo huo, inatakiwa kukodisha mtambo mwingine wenye uwezo wa kuzalisha megawati 150 haraka iwezekanavyo itakayotumika kwa miaka miwili.

Aidha, alishauri pia kuwa serikali inapaswa kutenga fedha haraka kwa ajili ya kujenga kituo cha kutumia mafuta mazito mkoani Mwanza na pia iingilie ujenzi wa mradi wa Kiwira utakaozalisha megawati 200 ili uweze kukamilika mapema.

Alisema mipango ya serikali ya kujenga vituo vipya vya kuzalisha umeme kikiwemo cha Rufiji kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha megawati 358, Kinyerezi megawati 240 na Kiwira megawati 200 haitafanikiwa kuondoa tatizo la umeme kwa kuwa vituo hivyo havitaweza kukamilika katika kipindi cha mwaka huu na 2013.

Aidha, alisema mipango iliyopo sasa ni kujenga kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia gesi asilia cha Tegeta, Dar es Salaam ambacho kitamalizika Oktoba mwaka huu, Kinyerezi, kituo cha kutumia mafuta mazito mkoani Mwanza, kituo cha kutumia makaa ya mawe cha Kiwira, kituo cha kutumia upepo mkoani Singida na cha Mnazi Bay.

Serikali inataka kununua mitambo hiyo kwa gharama ya Sh. bilioni 70.

Mbali ya kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kupinga maamuzi ya ununuzi huo, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyochunguza mkataba tata wa Richmond/Dowans, Dk. Harrison Mwakyembe naye amepinga.

Wakati wadau hao wakipinga, Kamati ya Bunge ya Hesabu za mashirika ya Umma, kupitia kwa Mwenyekiti wake, Kabwe Zitto, inaunga mkono ununuzi huo.

Aidha, hatua hiyo, imeibua mvutano baina ya kamati ya Bunge ya Nishati na Madini na hiyo ya Mashirika ya Umma, pamoja na wanasiasa mbalimbali.

Naibu Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Dk Wilbroad Slaa, amekaririwa mara kadhaa akipinga uamuzi huo na kuonya kwamba suala hilo linapaswa kuzingatia maslahi ya taifa.

No comments: