Ajali zaua 15 Dar na Moro
Watu 15 wamefariki dunia na 23 wamejeruhuiwa, baadhi yao vibaya, katika ajali za magari na treni zilizotokea jijini Dar es Salaam na Morogoro.
Akizungumzia ajali ya Dar es Salaam, Kamanda wa Polisi wa Ilala, Faustine Shilogile, alisema ajali hiyo ilitokea eneo la Jeti, katika barabara ya Nyerere jana asubuhi na kuua watu tisa na kujeruhi 13.
Alisema ajali hiyo ilisababishwa na lori aina ya Scania lililokuwa limebeba mchanga lilipoingia barabara ya Nyerere katika eneo hilo bila kuchukua tahadhari.
Alisema wakati lori hilo lenye namba za usajili T 452 na trela lenye namba za usajili T 442 ACP likingia barabara kuu, liligongana na lori la mchanga aina ya Mitsubishi Fuso, lenye namba za usajili T 334 AHD lililokuwa likiendeshwa na Leonard Wilson likitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere likielekea eneo la Tazara.
Alisema baada ya magari hayo kugongana, lori aina ya Fuso lilipinduka na kuangukia upande wa pili wa barabara na ndipo daladala aina ya Toyota Hiace yenye namba za usajili T 700 AST iliyokuwa ikitokea Ukonga kwenda eneo la Tazara, ikaligonga trela la Scania na kisha ikaingia uvunguni mwake.
Wakati ajali hiyo ikitokea Dar es Salaam, watu sita waliodandia treni walifariki na wengine kumi kujeruhiwa baada ya mabehewa mawili yenye mataruma ambako walikuwamo, kuacha reli na kuanguka eneo la Kilosa mkoani Morogoro.
Treni hiyo ya Kampuni ya Reli (TRL) ilikuwa imebeba mataruma yaliyoharibika yakitolewa Dodoma kwenda Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa taarifa ya TRL, behewa moja la abiria 68 kutoka Mpanda, mkoani Rukwa, ambalo lilikuwemo katika treni hiyo iliyopata ajali haikupata madhara yoyote ya abiria wote walikuwa salama.
Taarifa hiyo inafafanua zaidi kwamba behewa hilo kwa kawaida hutumika kutoa huduma baina ya stesheni za Mpanda na Tabora, hata hivyo, utaratibu maalum ulitumika kuwasafirisha abiria hadi Dar es Salaam, baada ya kukwama katika Stesheni ya Tabora.
Akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu kutoka katika eneo la tukio, Kamanda wa Polisi Kikosi cha Reli,Yessaya Msigwa, alisema kuwa ajali hiyo ilitokea majira ya saa saba usiku wa kuamkia jana.
Alisema kuwa ajali hiyo imehusisha treni yenye namba 8828 iliyokuwa ikitokea Bara kuelekea jijini Dar es Salaam ikiendeshwa na Richard Mkude (38) na msaidizi wake, Lucas Isaya, wote wakazi wa Morogoro.
Aliwataja waliokufa katika ajali hiyo kuwa ni wafanyabiashara ambao ni Said Pindupindu, Seif Bakar, Nassoro Mohamed, Jonas Lukanda na Abbas Kandaro kutoka Kilosa na mwingine ambaye hajatambuliwa jina.
Waliojeruhiwa katika ajali hiyo na kulazwa katika Hospitali ya wilaya ya Kilosa ni pamoja na Hamisi Chamwitu, Seleman Mohamed, eradic Monera, Easter Mbwambo na Asha Khamis wakazi wa Morogoro; Edward Athanas na Aziz Seleman wa Dar es Salaam.
Wengine ni Hamis Manyeleta, Hamis Selemani, Mecha Jackson, wakazi wa Kilosa na kwamba maiti na majeruhi wamepelekwa katika Hospitali ya wilaya ya Kilosa.
Hata hivyo, alisema kuwa zoezi la kutambua maiti hao lilikuwa likiendelea ambapo watano kati yao walitambuliwa na ndugu zao na majeruhi wanaendelea vizuri baada ya kupatiwa matibabu katika hospitali hiyo.
Mkuu wa Wilaya ya Kilosa, Athuman Mdoe, pamoja na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Thobias Andengenye, walithibitisha kutokea kwa ajali hiyo.
No comments:
Post a Comment