Baada ya kuyumba kuhusu mapambano dhidi ya ufisadi mwaka juzi na kujikuta akimtetea aliyekuwa Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Daudi Ballali, Mbunge wa Kwela, maarufu kama `mzee wa mabomu`, Chrisant Mzindakaya, jana aliibuka na kumlipua Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga, kwa kukiuka azimio la Bunge.
Bomu hilo alilolitoa kama hoja binafsi, lilimpa wakati mgumu Waziri Mangunga ambaye alijishusha na kuliomba radhi Bunge na kujiunga na kauli za serikali za kuomba radhi bungeni baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kuchukua hatua kama hiyo juzi.
Pinda aliiomba radhi Bunge na Watanzania kutokana na kauli yake ya kutaka wauaji wa maalbino nao wauawe, aliyoitoa akiwa katika ziara ya Kanda ya Ziwa.
Pinda aliomba radhi huku akitokwa machozi katika kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu.
Mzindakaya akiwasilisha hoja yake kwa ustadi mkubwa, alimbana Waziri Mangunga kutokana na hatua yake ya kuupuza azimio la Bunge la kutaka kufutwa kwa muda wa umiliki wa vitalu vya uwindaji wa kitalii na badala yake akaongeza muda hadi mwaka 2012.
Mbunge huyo alimfikisha waziri katika hali hiyo baada ya kueleza jinsi alivyokaidi azimio la Bunge na kupendekeza pamoja na mambo mengine kukemewa kwa Waziri Mwangunga.
Mzindakaya yekumbukwa kwa kuibua `mabomu` mbalimbali yaliyowatikisa vigogo wa serikali hata baadhi yao kufikia kujiuzulu, kama alilomlipua aliyekuwa Waziri wa Kwanza wa Fedha wa Serikali ya Rais Benjamin Mkapa mwaka 1996, Profesa Simon Mbilinyi, aliyejiuzulu, aliitaka serikali kufuta mara moja barua ya Wizara ya Maliasili na Utalii yenye Kumb. Na. HD 204/401/100 ya Januari 16, mwaka huu.
Alisema barua hiyo ndiyo inayoongeza muda wa umiliki wa vitalu vya uwindaji kwa kipindi cha miaka mitatu hadi 2012 kwa kuwa inakwenda kinyume cha Azimio la Bunge.
Mzindakaya alisema kwa kuwa Waziri huyo hakulipa suala hilo mwongozo mzuri, Bunge linakemea tabia hiyo ambayo athari zake ni kuleta mtengano kati mihimili miwili ya Bunge na Utawala.
Pia alisema ili kujenga ushirikiano kati ya mihimili hiyo miwili, ni busara kwa wizara za serikali, kuzingatia mawasiliano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake.
Alisema kwa kuzingatia hali halisi ilivyo sasa na kwa kuwa wizara imechelewa utekelezaji wa Azimio la Bunge, utekelezaji wake ukamilike mwaka 2010 na siyo 2012.
Awali, katika hoja yake, Mzindakaya alisema katika mkutano wa Bunge wa 11, lilijadili hoja kuhusu ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa wanyamapori na bei zake ambavyo muda wake unaishia mwaka 2009.
Alisema baada ya kujadili hoja hiyo, Bunge liliazimia kwamba, ili kuiwezesha serikali kuongeza mapato na kuweka uwiano, uwazi na usawa katika ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa kitalii, serikali ianze mchakato wa kuvigawa upya vitalu vyote nchini ambavyo muda wake wa mwisho wa umiliki ni mwaka 2009 kwa kuzingatia mapendekezo yaliyowasilishwa bungeni.
Aliongeza kuwa kusudi la azimio hilo la Bunge lilikuwa ni vitalu vyote vya uwindaji nchini vigawiwe upya ili wamiliki wapya waanze kuvitumia mwaka 2010 baada ya muda wa awali wa vitalu kumalizika mwaka huu.
Lengo lingine alisema lilikuwa ni kuliwezesha taifa kupata mapato zaidi kutokana na shughuli za uwindaji wa kitalii wa wanyamapori kwa kuvigawa vitalu vikubwa na kupata vitalu vingine vipya 89 vilivyogawanyika katika madaraja mawili, yaani daraja la kwanza lenye vitalu 55 na la pili lenye vitalu 34.
Hata hivyo, Mzindakaya alisema pamoja na Waziri Mwangunga kuahidi kwa dhati bungeni kwamba, serikali ingezingatia na kutekeleza ipasavyo azimio lililopitishwa na Bunge ikiwa ni pamoja na kuandaa Muswada wa Sheria mpya wa Wanyamapori itakayosimamia shughuli zote za ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa wanyamapori, lakini ameamua kuongeza muda wa umiliki wa vitalu hivyo kwa miaka mitatu kwa utaratibu wa zamani.
Alisema utaratibu huo wa zamani unalitia hasara taifa kiasi cha Dola za Marekani 4,110,000 kwa mwaka ambapo kwa miaka mitatu, itasababisha hasara ya Dola za Marekani 12,330,000.
Mzindakaya alisema maelezo ya Waziri Mwangunga katika kauli yake aliyoitoa bungeni kwamba serikali ina makubaliano na Chama cha Wawindaji (TAHOA), hayana msingi wowote kwa kuwa makubaliano yalifanywa zaidi ya miaka ya 10 iliyopita siyo mkataba.
Alisema kitendo chochote cha serikali kuingilia kati mchakato wa utelekezaji wa azimio la Bunge kuhusu ugawaji wa vitalu vya uwindaji wa wanyamapori, kunaingilia madaraka ya Bunge na kukiuka haki za Bunge.
Akijibu hoja ya Mbunge huyo, Waziri Mwangunga alikiri kuwa serikali iliahidi kulifanyia kazi azimio la Bunge kwamba umiliki wa vitalu vya uwindaji vingeishia mwaka 2009.
Hata hivyo, Waziri Mwangunga alisema serikali haijadhrau azimio la Bunge bali kabla ya kufikia uamuzi huo, iliwasiliana na Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuelezea hali hiyo, kabla ya kufikia uamuzi wa kuongeza muda wa umiliki wa vitalu vya uwindaji.
Hata hivyo, Waziri huyo alilazimika kuliomba radhi Bunge kwa kosa hilo ambalo walidhani kwa kuwasiliana na kamati hiyo, ilikidhi haja ya kuwasiliana na Bunge.
Kwa msingi huo, Waziri Mwangunga alisema serikali iko tayari kukubali kufuta ugawaji wa vitalu hivyo kama hoja ya Mbunge huyo inavyotaka.
Hata hivyo, alitahadharisha kuwa, uamuzi huo unaweza kuleta athari kadhaa kwa taifa.
Alizitaja athari hizo kuwa ni pamoja na baadhi ya wadau kwenda mahakamani kudai sheria imekiukwa, watalii wawindaji kususia kuja Tanzania na kuongezeka kwa ujangili.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Kabwe Zitto, alisema kwa kosa hilo alilofanya Waziri ambalo ni la kudharau maazimio ya Bunge, wabunge wangeweza kuamua apelekwe gereza la Keko kwa siku saba.
``Alichokifanya Mheshimiwa kama tukiamua kuwa `serious` (makini), angekwenda Keko siku saba,`` alisema Kabwe huku akinukuu sheria ya madaraka na wajibu wa Bunge ya mwaka 1988.
Mbunge mwingine, Fred Mpendazoe (CCM-Kishapu), alisema Wizara ya Maliasili na Utalii, imekiuka na haikutekeleza azimio la Bunge bali imenufaisha watu wengine. Mpendazoe alisema utajiri wa Watanzania unaliwa na wageni kwa kushirikiana na Watanzania wachache.
Huku akirejea maandiko katika Biblia, aliitaka serikali kuhakikisha kwamba inawajibika kwa Bunge pasipo kusitasita.
Akizungumza kwa hisia kali, Mbunge huyo alisema vurugu nyingi ambazo hutokea duniani, husababishwa na viongozi waliopewa dhamana na wananchi kwa kuona kwamba madaraka waliyopewa na wananchi ni ya kujinufaisha badala ya kuwasaidia wananchi waliowaweka madarakani.
Aliwataka Watanzania kubadilika na kutooneana haya na kwamba kipindi kijacho ikitokea kiongozi wa serikali akakiuka maazimio ya Bunge, hakuna haja ya kwenda bungeni kutoa maelezo badala yake aende akiwa na barua ya kujiuzulu.
Hata hivyo, Spika wa Bunge, Samuel Sitta, baada ya kuona mjadala huo unaelekea kuchukua muda mrefu, alilazimika kuingilia kati kwa kumtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kutoa ufafanuzi wa kauli ya Waziri Mangunga juu ya muda wa kukoma kwa vibali hiyo kwa kuwa yeye (Pinda) ndiye mwenye dhamana ya serikali bungeni.
Pinda alisimama na kueleza kwamba serikali imekubaliana na azimio la Mzindakaya la kufuta barua hiyo, pamoja na athari zitakazotokea.
Kutokana na ufafanuzi wa Pinda na hasa baada ya Waziri Mangunga kuomba radhi, Sitta aliwashauri wabunge kwamba, maadam Waziri amekuwa muungwana na kuomba radhi na kukubali kufuta barua ya umiliki wa vitalu, ni vema mjadala ukaisha kwa kuamua juu ya hoja hiyo.
Mtoa hoja, Mzindakaya, alikubaliana na Spika na kutokana na Waziri kuomba radhi, alikubali kuondoa moja ya maazimio yake manne na kubakia matatu.
Azimio aliloliondoa ni lile la Bunge kukemea tabia iliyofanywa na Waziri Mwangunga ambayo athari zake zinaweza kuleta mtengano kati ya Bunge na Utawala.
Kwa hatua ya jana, Mzindakaya amerejesha heshima yake iliyokuwa imeyumba mwaka juzi baada ya kumtetea Balallali wakati moto wa ufisadi ndani ya BoT ulipoibiliwa bungeni na Mbunge wa Karatu (Chadema), Dk. Willibrod Slaa.
Kombora la Dk. Slaa ndilo lilikuja kuibua sakata la Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) likiwa linatikisa kila kona ya nchi kwa sasa.
Tayari watu 21 wameshitakiwa kwa EPA baada ya kuhusika na wizi wa Sh bilioni 133.
Saturday, January 31, 2009
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment